ECOWAS Yaomba Isaidiwe Mali

Tuesday, January 22, 2013

VIONGOZI wa nchi za Afrika magharibi wameomba msaada wa kimataifa kugharimia majeshi yao kuingilia kati nchini Mali. Walisema hayo kwenye mkutano unaofanywa Abidjan, Ivory Coast. Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, ambaye amehudhuria mkutano huo, ameshikilia kuwa majeshi ya Afrika yatashika uongozi wa operesheni za kijeshi nchini Mali katika majuma yajayo. Nchi kadha za Afrika Magharibi zimeahidi kujitolea kwa wanajeshi ili kulisaidia jeshi la Ufaransa katika mapambano yake dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu, lakini nchi hizo zina shida za usafiri na fedha na hivo zinaweza kuchelewa kutuma wanajeshi wao Mali. Hata hivo, Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, amesisitiza kuwa majeshi ya Afrika yatachukua nafasi ya Ufaransa katika majuma tu yajayo. Lakini uwezo mdogo wa wanajeshi wa Afrika Magharibi kushiriki kwenye vita kaskazini mwa Mali huenda ukaifanya Ufaransa ilazimike kubaki vitani kwa miezi kadha ijayo. Wanabalozi wa mataifa ya magharibi wanasema kuwa kisa cha wageni kutekwa nchini Algeria, kimeyafanya mataifa makuu kuamini kuwa lazima yapambane na makundi ya wapiganaji wa Kiislamu yalioko kaskazini mwa Mali. -BBC

2013 muziki wa kizazi kipya uwe wa ubunifu zaidi

SANAA ya muziki Tanzania imekuwa ikikua siku hadi siku. Moja ya viashiria vya kukua kwa muziki ni kuibuka kwa wanamuziki kila kukicha ambao wamekuwa wakija na staili tofauti kwa lengo la kukamata soko la ndani na nje ya nchi. Kuna waliofanikiwa kufanya vizuri na kukamata soko la ndani na nje na kufanya mambo muhimu na hata kutengeneza mazingira ya kutoa ajira kwa Watanzania wenzao. Lakini pia kuna walioishia katika soko la hapa nyumbani na hakuna lolote la maana walilofanya zaidi ya kulewa sifa na umaarufu. Halikadhalika kuna walioshindwa kutimiza ndoto zao katika fani hii ya muziki lakini bado wanaendelea kujaribu bahati yao. Moja ya aina ya muziki ambao umekuwa unajaribiwa na wengi na hasa vijana ni ule muziki wa kizazi kipya, maarufu kama Bongo fleva. Kwa wale wapenzi wa burudani ya muziki watakubaliana na mimi kuwa aina hii ya muziki imekuwa ya majaribio kwa kila kijana ambaye anajisikia kuwa anaweza kuingia katika tasnia ya muziki. Hivi karibuni tumeshuhudia hata watu wazima wenye umri wa miaka zaidi ya 50 nao wakitupa karata yao katika aina hiyo hiyo ya muziki. Haya yote yamefanyika na kweli wapo waliofanikiwa kuufanya muziki wa Bongo fleva vizuri kwa kujipatia mashabiki wengi na hatimaye kupata soko. Katika miaka ya nyuma wanamuziki wa Bongo fleva walikuwa wanaweza kufanya maonyesho mengi zaidi ikiwepo yale ya uzinduzi wa albamu tofauti na ilivyo sasa. Kinachofanyika sasa hivi katika muziki wa kizazi kipya ni wanamuziki kufanya nyimbo zao kwa kushirikishana. Hali hii ambayo inatafsiriwa kama njia ya kutafuta soko na umaarufu kwa nguvu inafanywa zaidi na wale wanamuziki wanaochipukia kwa kuwashirikisha wale wakongwe na hasa wenye majina makubwa. Kwa harakaharaka, tafsiri yake ni kwamba wanamuziki wanaochipukia kwa sasa katika muziki wa kizazi kipya hawawezi kusimama wenyewe na kuleta mabadiliko bali wameona njia pekee ya kulazimisha soko ni kuwashirikisha wanamuziki wenye majina makubwa. Hii ni mojawapo ya viashiria kwamba kumbe muziki wa kizazi kipya hauna ubunifu kama ilivyo katika aina nyingine ya muziki kama vile dansi na nyinginezo. Kuna wanamuziki waliokuwa wakipiga Bongo fleva zamani na sasa wamegundua kuwa muziki huo sasa hauna jipya na sasa wameamia katika staili nyingine na pia wengine wameamua kuanzisha bendi zao ili kupiga muziki wenye ladha tofauti. Huu ni uamuzi mzuri ambao unakwenda na wakati na hasa katika karne hii ambayo imejaa uvumbuzi na ushindani wa kila aina. Kuna kundi jingine la wanamuziki wa muziki wa kizazi kipya ambao wamepotea katika macho na masikio ya wadau wa muziki japokuwa waliwika sana enzi hizo. Aidha pia kuna wale ambao ubunifu wao ni kama umefika kikomo na kilichobakia ni kupata mashabiki kwa sababu wana mvuto kwa wapenzi wa muziki wa aina hiyo, na hii ni kwa sababu kila wakipanda majukwaani nyimbo wanazoimba ni zile zile za miaka nenda rudi. Hili nalo limeleta mjadala kwani kuna wanaothubutu kusema kuwa bora Bongo fleva ya zamani ni bora kuliko ya sasa. Wanaosema haya wana sababu kuu ya msingi ya kwamba Bongo fleva ya sasa haidumu sokoni kama ilivyokuwa ya miaka ile kwa sababu wasanii wa sasa hawawezi kufanya muziki bila kuwashirikisha wasanii maarufu. Kwa maana hiyo ni kwamba kama wasanii wanaochipukia watashindwa kusimama imara hakutakuwa na jipya katika Bongo fleva kwa miaka ijayo. Mfano mzuri ni katika mojawapo ya onyesho la Krismasi lililofanyika wiki iliyopita katika moja ya kumbi maarufu za jijini Dar es Salaam. Katika onyesho hilo kulikuwa na wasanii wa muziki wa Bongo fleva wa sasa na wa zamani. Kilichotokea ni kwamba wale wanamuziki wa sasa na wale wakongwe wa Bongo Fleva wote walipokelewa kwa shangwe sawa na mashabiki waliokuwa wamefurika katika ukumbi huo. Halii hii ilitafsriwa kama ule usemi usemao kuwa ‘Ya kale ni dhahabu.’ Hii ikiwa na maana ya kwamba bado wanamuziki wakongwe katika Bongo fleva wana nafasi kubwa ya kukubalika kuliko wa sasa. Tatizo kubwa la wanamuziki wa sasa wamelewa sifa na umaarufu na wengine kutumia nafasi hiyo kuendekeza mapenzi kwa kubadilisha wasichana kama nguo. Hawa nao wamejisahau bila kujua kuwa kuna wasanii wengi wa tabia kama hizo walishapita na sasa wana maisha magumu na kilichobaki masikioni mwa watu ni historia tu. Mwaka 2013 uwe wa mabadiliko kwa wanamuziki wa Bongo fleva kwa kuja na ubunifu zaidi kwa sababu kwa sasa hali ilivyo Bongo fleva ni kama Big G inayotafunwa na baadaye kuisha utamu. Ni muziki ambao unadumu kwa muda mfupi na kupotea kabisa katika macho na masikio ya mashabiki. Sababu kubwa ni wasanii kutojiandaa kabla ya kutengeneza nyimbo zao. Tabia hii ya wasanii wa Bongo fleva ya kufanya nyimbo zao bila kujiandaa imewaingiza katika wimbi la kuiga, yaani Kukopi na kupesti. Hali inaonyesha kuwa wanapenda njia ya mkato zaidi kuliko kubuni stahili zao. Wanamuziki wa Bongo fleva sasa wamekumbwa na upepo wa Afrika Magharibi na Afrika Kusini. Hali hii ya kuiga imetawala sana katika mwaka 2012 ambapo tumeshuhudia wanamuziki wengine wakipata tuzo za ubora kutoka kwa waandaaji wa mashindano mbalimbali ya muziki. Hali hii pia ilileta maswali mengi kwa waandaaji wa tuzo hizo, swali kubwa likiwa ni kwamba ni vigezo gani wanavyovitumia kupata washindi wa tuzo hizo. Tabia ya kupenda kuiga bila kujifunza pia imeshuhudia wanamuziki wetu wakijaribu kuimba nyimbo zao moja kwa moja kwa kufuatisha vyombo majukwaani, lakini bado kiwango chao kinaonekana kuwa ni cha kuchechemea au dhaifu. Mfano mzuri ni katika mojawapo ya tamasha kubwa la muziki ambalo limekuwa likifanyika kila mwaka katika sehemu mbalimbali hapa nchini na kujizolea umaarufu. Mwaka jana Nilishuhudia wanamuziki wa muziki wa Bongo fleva wakijaribu kuimba na vyombo, yaani Live. Kwa wale wanaofahamu uimbaji wa staili hiyo watakubaliana na mimi kuwa vijana hao ambao ni maarufu katika muziki wa Bongo fleva kuwa ‘walichemka’ hivyo kuwashangaza watu wengi. Ndiyo, kujaribu kufanya kitu anachofanya mwenzio si vibaya, lakini pia kabla ya kujaribu ni vyema kufanya maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti za hapa na pale kufahamu kuwa wale ambao walifanya hivyo na kufaulu walitumia njia zipi hadi kufikia mafanikio. Wanamuziki wa Bongo fleva hawanabudi kutambua kuwa kuteleza siyo kuanguka, kwa hiyo bado wana nafasi ya kuangalia ni wapi wameteleza na kujirekebisha na hatimaye kufanya vizuri zaidi. Nina imani kuwa kuna Watanzania wengi ambao wangependa kuona mabadiliko katika muziki wa kizazi kipya kuliko kuona kila siku wakiiga staili kutoka nchi za Magharibi ambazo mwisho wa siku zitachangia kumomonyoa maadili yetu na kufunika utamaduni wetu. Wanamuziki wa Bongo fleva kama walivyo wasanii wengine, wana haki ya kutangaza utamaduni wao kama mojawapo ya wajibu wa msanii wa aina yoyote ile. Mwaka 2013 Bongo fleva iwe ya ubunifu zaidi na hili bado linawezekana.

Kombe la Mapinduzi liamshe soka la Zanzibar

MICHUANO ya mpira wa miguu ya Kombe la Mapinduzi iliyoisha wiki iliyopita katika kilele cha sherehe za mapinduzi mjini Unguja katika uwanja wa Aman, kwa timu ya Azam FC kutetea taji imenipa mwanga mkubwa katika soka la visiwani humo. Kwa hakika nimeshuhudia soka la uhakika katika michuano ile hasa kutoka timu za visiwani, lakini katika kila timu wenyeji yaani za visiwani kulionekana kasoro moja tu ya uzoefu kwa wachezaji wake. Miembeni, Jamhuri ya Pemba ambao ndiyo mabingwa wa soka Zanzibar na Bandari ndiyo timu wenyeji zilizoshiriki michuano hiyo. Lakini Miembeni ndiyo iliyofanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ikitolewa na Tusker FC ya Kenya. Kwa soka waliloonyesha Miembeni na Jamhuri ya Pemba nimevutiwa kutaka kuwaona wakiendelea zaidi na zaidi. Maana ya maneno haya ni kuwashawishi viongozi wa timu mbili hizi kuomba mechi nyingi za kirafiki na timu za Tanzania Bara ima kwa kuzialika au wao kuzifuata kila msimu wa ligi kuu unapoisha. Nimefuatilia kwenye kumbukumbu nimeona Miembeni ni timu kongwe kuliko hata baadhi ya timu zinazoonekana bora katika ligi kuu ya Tanzania Bara, Miembeni ilianzishwa mwaka 1945. Katika mafanikio yao tangu kuanzishwa Miembeni walishachukua ubingwa wa ligi kuu Zanzibar mwaka 1987, 2007 na 2008. Halafu katika kombe la Mwalimu Nyerere wamechukua mara tatu mwaka 1985, 1986 na 1987. Kikombe cha Mapinduzi wamechukua mara mbili mwaka 2008 na 2009. Aidha Miembeni FC walishiriki kombe la shirikisho (CAF) mwaka 2010, wakashiriki kombe la mabingwa barani Afrika (African Cup Winners) mwaka 1986, 1987 na mwaka 1988. Si mafanikio madogo kwa timu ambayo watu wengi hawaijui ama wanaijua lakini hawaitilii maanani. Timu ya pili kutoka visiwani humo ambayo ilinivutia ni Jamhuri ya Pemba, hawa ni mabingwa wa ligi kuu Zanzibar kwa msimu uliopita mwaka 2012. Ilianzishwa mwaka 1953 ikiwa na makazi yake mjini Wete Pemba. Wao wamechukua Kombe la Mapinduzi mara moja yaani mwaka 1998, na mwaka 2012 walifika fainali wakafungwa na Azam FC. Jamhuri ya Pemba iliushangaza umma kwa kuifunga Mtibwa Sugar magoli manne kwa moja (4-1) katika mechi ya ufunguzi wa kundi B michuano ya Mapinduzi iliyomalizika juzi. Ina kikosi bora kinachoweza kuleta ushindani katika soka la Afrika, lakini macho mangapi yanashuhudia uwezo huo? Lengo la makala haya ni kuwafungua macho viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kuzitangaza zaidi timu zao kwa kupitia michuano mikongwe kama hii ya Mapinduzi. Historia inaonyesha mwisho wa michuano ya Mapinduzi wachezaji wa timu za Zanzibar wanaishia kuchukuliwa na timu zilizoalikwa. Hiyo si sifa wala jambo la kujivunia maana kuchukuliwa wachezaji ina maana moja tu ambayo ni kudhoofisha soka la Zanzibar. Vijana wa Zanzibar wanapenda kucheza soka, lakini wanaonekana kurudishwa nyuma na mifumo mibovu ya viongozi wao. Suala la viwanja bora vyenye viwango na mikakati ya vyanzo vya mapato kwa timu hizo ni kitu cha kuzingatia sana. Dunia sasa inaendeshwa kwa ujasiriamali katika michezo, biashara nyingi zinatangazwa na vilabu vya mpira wa miguu. Uchumi wa Zanzibar unaweza kukua kwa kutegemea soka ikiwa wataweka mbele malengo ya wachezaji wao.

Matangazo ya AFCON katika tv yazua mgogoro

MALALAMIKO yameanza kujitokeza katika maandalizi yanayoendelea ya michuano ya klabu bingwa Afrika (Afcon) itakayofanyika nchini Afrika Kusini, ambako tayari timu za mataifa yanayoshiriki michuano zimekwishaweka kambi. Tayari Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utangazaji nchini Nigeria (BON), Alhaji Abubakar Jijiwa, amelalamikia utozaji mkubwa wa hatimiliki kwa chombo cha habari kinachotaka kurusha matangazo hayo ya soka. Taarifa zinaeleza ya kuwa malalamiko hayo yanajitokeza katika wakati ambao michuano ikiwa imefadhiliwa kwa karibu kila nyanja na wafadhili wakubwa Ni kutokana na ufadhili huo Jijiwa anahoji, kama michuano imefadhiliwa kwa kiasi hicho ni kwa nini wao watozwe fedha nyingi? Na kwa hiyo anasema; "Mashirika ya utangazaji Nigeria tumekataa kulipa Euro milioni nane kwa ajili ya haki ya chombo cha habari kurusha matangazo hayo, tunasikitika kwa Wanigeria kutoweza kuangalia matangazo haya kama walivyotaraji."

Kova ataka usalama hosteli za IFM

SIKU chache baada ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kufanya maandamano, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleman Kova, amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englbert Kiondo, kusimamia usalama wa hosteli za wanafunzi hao zilizoko Kigamboni. Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Kova alisema amelazimika kutoa agizo hilo baada ya kuwepo kwa mvutano kati ya Kiondo na wanafunzi hao ambao walidai taarifa zote za uhalifu walizofanyiwa na kundi la vibaka kwenye hosteli zao zimeripotiwa katika kituo kidogo cha polisi Kigamboni. Naye msimamizi wa hosteli mojawapo, aliyefahamika kwa jina la Sanfroza alieleza wazi kuwa anashangazwa na ripoti ya polisi kuwa matukio ya vitendo hivyo hayako katika orodha kwa sababu yote yameripotiwa ipasavyo. “Tunachotaka sisi kwa sasa ni jeshi la polisi kuwajibika katika vitendo vyote vya uhalifu vilivyotokea hosteli, kwa sababu majina ya vibaka wote yameripotiwa polisi Kigamboni, iweje leo warushiane mpira wenyewe kwa wenyewe?” alihoji Sanfroza. Wanafunzi hao walifanya maandamano Januari 14, mwaka huu, ambapo Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kiliingilia kati kwa kuwatawanya kwa mabomu ya machozi. Pamoja na hilo, Kova aliahidi kutoa ufafanuzi wa matukio hayo wakiwemo vibaka waliohusika wawe ndani ya Dar es Salaam au nje ifikapo Januari 30, mwaka huu.

Ukuta waharibu magari 19 Ubungo

UKUTA wa kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo jijini Dar es Salaam (UBT), umeanguka ghafla na kujeruhi watu wanne huku magari madogo 19 na pikipiki za matairi matatu (bajaji) vikiharibika vibaya. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha tukio hilo akisema kuwa lilitokea alfajiri saa 12 jana, kutokana na ukuta huo kuelemewa upande mmoja baada ya kubomolewa upande mwingine. Kenyela alisema hakuna aliyepoteza maisha, isipokuwa watu wanne walijeruhiwa na kupatiwa matibabu hospitalini, na juhudi za kutoa magari hayo zilikuwa zikiendelea. Magari yaliyoharibika yalikuwa yameegeshwa jirani na ukuta huo na watu waliokuwa wamewasindikiza ndugu zao kupanda mabasi kituoni hapo. Hata hivyo, pamoja na ukuta huo kubomolewa upande mmoja juzi, uongozi wa kituo hicho haukuweka alama yoyote ya kuwatahadharisha watembea kwa miguu wala wenye magari wasisogelee eneo hilo. Kwa mujibu wa kamanda Kenyela, magari yenye bima wamiliki wake watarudishiwa gharama zote baada ya kufanyiwa tathmini. Nao mashuhuda wa tukio hilo, waliliambia Tanzania Daima kuwa chanzo ni uzembe wa mkandarasi pamoja na meneja wa kituo hicho. Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika eneo la tukio, wananchi hao walisema kuwa serikali inapaswa kulaumiwa kwa kutofanya maandalizi ya kutosha kabla ya kubomoa. Mashuhuda hao walisema kuwa licha ya ujenzi kuendelea, askari wa wanaolinda humo ndani walikuwa wakiendelea na utaratibu wa kutoza fedha za maegesho na kuwaelekeza madereva eneo kuegesha eneo hilo la ukuta. Naye meneja wa kituo hicho, Idd Juma, hakutaka kuzungumza chochote kwa madai kuwa si msemaji na hivyo kutaka asubiriwe mkurugenzi wa manispaa hiyo. Akizungumzia ajali hiyo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema wakati hatua za kisheria zikitakiwa kuchukuliwa haraka kutokana na uzembe uliosababisha tukio hilo serikali kuu inapaswa kuingilia kati kuepusha maafa zaidi. Akizungumza kituoni hapo, Mnyika alisema ajali hiyo ya kizembe ni matokeo ya udhaifu wa serikali kutochukua hatua kwa wakati, hivyo inatumia utaratibu mbovu kukihamisha huku kikiendelea kutumika. “Tangu 2011 niliishauri serikali, ikiwemo kupeleka hoja binafsi kwenye Baraza la Jiji, ambapo pamoja na masuala mengine, niliitaka kufanya maamuzi ya haraka kuainisha mapema maeneo ya kituo cha basi Ubungo, ambayo yatatumia mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART),” alisema. Alisema kuwa kwa mwenendo huo wa kuitegemea menejimenti ya kituo kutokana na sh milioni 5 inayokusanya kila siku hapo, hawatamaliza kujenga hicho kituo mapema, hivyo wito kwa Rais Jakaya Kikwete ili fedha zitoke kituo kipya kijengwe.

POSITION: HR OFFICER(1)

Qualification; Degree holder in HRM or related field from a recognized institution;- Experience: Working in the senior position with reputable organization at list (3-5) years’ experience in the related field. Specialized on retail business with numerous branches, managing at list 300/500 employees with staff ratio 1/3 cashiers, sell persons, bouncers. POSITION; PERSONAL ASSISTANT (1) QUALIFICATION: Degree holder in Public administration/Business administration/Law or other related field. EXPERIENCE:Working as senior in the same position at list 5 years with an international reputable organization. 1) POSITION:CASHIER (20) QUALIFICATIONS: - EDUCATION: A LEVE/O - LEVEL SECONDARY EDUCATION - CERTIFICATE IN ACCOUNTING ECONOMICS FINANCE BUSNESS ADMINISTRATION SOCIAL SCIENCE OR RELATED FIELD WILL BE AN ADDEDADVANTAGE. - GOOD MATHEMATICAL BACKROUND - WORKING EXPERIENCE: PRIOR WORKING EXPERIENCE IN BANKING/MICROFINANCE EXPERIENCE OR SMALL ENTERPRICES WOULD BE AN ADDED ADVANTAGE. - COMPUTER LITERATES - GOOD MATHEMATICAL BACKGROUND - LANGUAGE – FLUENT IN ENGLISH AND SWAHILI. Deadline: 28th January 2013 HOW TO APPLY:ALL APPLICATIONS SHOULD BE SENT TO: lotusvalley468@yahoo.com or send to: HR MANAGER LOTUS VALLEY (T) LTD P.O.BOX 80496 Dar es Salaam.

Pinda kufungua kikapu

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda atafungua pazia la michuano ya mpira wa kikapu ya Kanda ya Tano itakayoanza saa 3 asubuhi kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Mussa Mziya aliliambia gazeti hili jana kuwa Waziri Mkuu Pinda atashiriki katika zoezi la ufunguzi litakaloanza saa 10 jioni uwanjani hapo. “Mashindano rasmi yataanza saa tatu asubuhi na ufunguzi utafanyika jioni saa kumi,” alisema Mziya na kuongeza kuwa maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika. Katika michuano hiyo inayoshirikisha mataifa ya Ukanda wa tano, Tanzania itawakilishwa na timu ya wanaume na wanawake, ambapo kocha wa timu ya wanaume, Bahati Mgunda amesema wachezaji wake wapo tayari kwa michuano hiyo. Mgunda alisema licha ya kutojua wanaanza na timu gani, vijana wake wamejiandaa kukabiliana na timu yoyote ile na kusisitiza kuwa karibu nchi zote zinazoshiriki mashindano hayo wanajua uwezo wao. Katika mashindano hayo, pia wachezaji kutoka vyuo vya Marekani na klabu za Canada, Morocco, Angola na Mexico watachezea nchi zao. Nchi zinazotarajiwa kushiriki mashindano hayo ni Burundi, Rwanda, Djibouti, Misri, Kenya, Uganda, Somalia na wenyeji Tanzania. Katika hatua nyingine, wachezaji wa timu ya taifa ya mpira wa kikapu ya wanaume na wanawake wametishia kutokushiriki mashindano ya Kanda ya tano ya Afrika kama uongozi wa TBF hautawalipa posho zao. Katika kikao cha pamoja kilichofanyika jana katika Hoteli ya Traventine Magomeni, wachezaji wote wa timu hiyo wametoa muda wa mwisho wa viongozi wao kulipa posho zao kabla ya kuanza mashindano hayo. Wachezaji wa timu hiyo kabla ya kuingia kambini walikuwa wakilipwa posho ya Sh6,000 kwa siku wakiwa mazoezini, lakini baada ya kuingia kambini fedha hizo ziliondolewa kabisa. Mmoja wa wachezaji hao (jina tunalo) alisema kikubwa wanachodai ni posho zao na mavazi ya michezo ya kuvaa wakati wa ufunguzi. “Tumechoka, hatukupenda kuongea na mwandishi wa habari kuhusiana na matatizo ya timu ya taifa, lakini imebidi ieleweke hivyo na tunataka Watanzania waelewe hivyo,” alisema mchezaji huyo. Alisema,”inaonekana mchezo huu wa kikapu umeingiliwa na wanasiasa, ukiangalia hata ahadi zao walizozitoa kwa wachezaji nyingi hazijatimia.” Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa matatizo yote yamejitokeza kutokana na baadhi ya viongozi kujiweka pembeni na kumwachia kiongozi mmoja afanye kazi peke yake.

Gyan: Mama amenikataza kupiga penalti

NAHODHA wa Ghana, Asamoah Gyan amesema hatopiga penalti katika muda wa kawaida wa mchezo wakati wa fainali za Mataifa ya Afrika zitakazoanza kutimua vumbi nchini Afrika Kusini wiki ijayo. Mshambuliaji huyo mwenye miaka 27, alikosa penalti iliyowanyima Ghana nafasi ya kufuzu kwa nusu fainali ya Kombe la Dunia 2010 na akakosa tena kwenye nusu fainali ya Kombe la Afrika mwaka jana. Baada ya kitendo hicho mshambuliaji huyo alijikuta kwenye wakati mgumu kutoka kwa mashabiki na kusababisha ajiuzulu kuichezea timu ya taifa kwa muda, lakini sasa Gyan ameamua kutopiga kabisa penalti. “Nimeamua kutokuwa mpigaji wa penalti wa timu ya taifa,” alisema. “Wachezaji wengi mashuhuri wanakosa penalti kama Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Diego Maradona. Ikiwa siku yako mbaya utakosa. “Lakini nilishasema mwezi moja uliopita kuwa sitopiga tena penalti. Kabla ya mama yangu hajafariki mwezi Novemba aliniambia nisipige tena penalti.” Miaka miwili iliyopita Gyan alishindwa kufunga penalti dhidi ya Uruguay kwenye dakika za mwisho za mchezo wa robo fainali ya Kombe la Dunia, na kama wangeshinda mchezo huo basi Ghana ingekuwa nchi ya kwanza ya Afrika kufuzu kwa nusu fainali kwenye historia ya mashindano hayo. Pia, Februari 2012, Gyan alikosa penalti iliyoinyima nchi yake kufuzu kwa nusu fainali dhidi ya Zambia. Ghana itaanza kampeni zake kwa kucheza na DR Congo kabla ya kuivaa Mali na Niger zote zikiwa Kundi B.

Matunda ya Yanga Uturuki yajibu Taifa

IKICHEZA soka lenye ‘harufu’ ya Uturuki, Yanga jana iliwathibitishia mashabiki wake ilichojifunza Ulaya baada ya kuiogesha kichapo cha mabao 3-2 Leopards ya Afrika Kusini katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Yanga ilirejea nyumbani mwanzoni mwa wiki hii baada ya wiki mbili za kujifua nchini Uturuki ilikocheza mechi tatu, ikifungwa mbili na sare moja. Jana Yanga ilikuwa tofauti na ilivyozoeleka awali kufuatia kuonyesha soka lenye ‘taaluma’ na kuwapeleka puta Chui kutoka Bondeni. Ingawa mchezo huo ulipooza dakika 10 za mwanzo kutokana na kila upande kujaribu kumsoma mwenzake, ulianza kuchangamka ndani ya robo ya kipindi cha kwanza. Dakika ya 10, nusura Didier Kavumbagu atikise nyavu za Chui hao wa Bondeni kama siyo shuti lake kali kutikisa mwamba wa goli, huku pia akishindwa kufunga dakika ya 22 kufuatia shuti lake kuchezwa na kipa. Mbuyu Twite angeweza kufunga kwa upande wa Yanga katika dakika ya 25, lakini shuti lake la karibu na lango lilichezwa na kipa wa Leopards. Shambulizi lingine kali kwenye lango la Leopard lilifanywa dakika ya 52 baada ya wachezaji wa Yanga kushirikiana vizuri lakini wakaishia ‘kumpasia’ mpira mkononi kipa. Leopards wangeweza kusawazisha bao hilo baada ya shuti la Rodney kugonga mwamba wa Yanga dakika ya 24, na akashindwa kufunga tena dakika ya 33 baada ya Ally Mustapha kudaka shuti lake. Leopards walirejea na kasi kipindi cha pili na kufunga bao la kusawazisha kupitia kwa Humphery Khoza akiunganisha kona ya Abbas Amidu, na kisha kufunga bao la pili dakika ya 88 kwa mkwaju wa penalti kupitia Romagalela baada ya Nadir Haroub kumwangusha ndani ya eneo la hatari Khoza. Frank Domayo aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 63 akimalizia pasi ya Niyonzima, kabla ya Tegete kufunga bao la tatu kwa shuti kali akiwa nje ya 18. Tegete aliyeng’ara safari ya Uturuki, aliipeleka Yanga mapumziko ikiwa mbele baada ya kufunga bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 33. Kiki hiyo ya penalti ilitolewa na mwamuzi baada ya beki wa Leopards, Nkoyiyabu Xakane kumfanyia madhambi Niyonzima ndani ya eneo la hatari. Kocha Ernets Brandts aliwapumzisha, mapacha Twite na kipa Mustapha na Tegete na kuingia Msuva, Juma Abdul, George Banda na kipa, Said Mohamed. Wakati huohuo, Mkutano wa wanachama wa klabu ya Yanga, ufanyika leo kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay Dar es Salaam huku ajenda kuu ikiwa kuzungumzia mapato na matumizi ya klabu. Yanga ilikuwa katika mgogoro wa uongozi kabla ya kufanya uchaguzi wake Julai 15 mwaka jana. Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema jana kuwa, mkutano huo utaanza saa 3:00 asubuhi na kusisitiza wanachama wanapaswa kuwahi ili kwenda na muda. Kizuguto alisema miongoni mwa mambo watakayozungumzia pia ni ushiriki wa timu yao wakati mzunguko wa pili wa ligi kuu ukikaribia. Ligi Kuu inatarajia kuanza Januari 26. Pia ajenda ya mengineyo itakuwa kufahamu idadi ya wanachama hai waliolipia kadi zao kwa wakati.

Mwakalebela amvaa Bayi TOC

Monday, January 21, 2013

KATIBU Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela amejitokeza kuwania nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC). Mwakalebela alichukua fomu hiyo jana asubuhi na kuijaza na kuirudisha muda huohuo ili aweze kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho ambacho uchaguzi wake umepangwa kufanyika Desemba 8, mjini Dodoma. Akizungumza na Mwananchi mara baada ya kurejesha fomu hizo, Mwakalebela alisema,"Kuna wadau wamenifuata na kuniomba nigombee, nimejitathmini na nimeona ninatosha hivyo nimeamua kula sahani moja na Bayi," alisema Mwakalebela. Alisema,"Ninajiamini na nimejipanga vya kutosha, najua Bayi ni kama Mbuyu TOC na mimi naingia kwa mara ya kwanza, nina wakati mgumu, lakini naamini mambo yatakwenda vizuri," alisema Mwakalebela ambaye amerejea jijini juzi akitokea Dodoma alipokuwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM. Mbali na Mwakalebela pia mwanariadha wa zamani Seleman Nyambui naye ametajwa kuwania nafasi ya Ujumbe ndani ya kamati hiyo. Hadi juzi jioni nafasi ya Katibu Mkuu ilikuwa na mgombea mmoja ambaye ni Filbert Bayi anayetetea nafasi yake na Rais wa TOC, Ghulam Rashid anayetetea pia nafasi yake hiyo. Wengine waliojitosa na nafasi zao kwenye mabano ni Hamis Abdul (Rais), Henry Tandau ambaye anawania nafasi ya Makamu wa Rais. Tandau pia alikuwa Mjumbe wa TOC na mkufunzi wa michezo nchini ambaye atachuana na Hassan Jarufu. Wengine waliojitokeza ni Jamali Idd (Katibu Msaidizi), Charles Nyange, Juma Hamis (Mweka Hazina Mkuu), wakati nafasi ya Mweka Hazina msaidizi inawaniwa na wagombea 16 ambao ni Irene Mwasanga, Linah Kessy, Nasra Juma, Mharami Mchume, Salum Salum, Noolain Sharif, Peter Mwita, Zakaria Gwandu, Suleiman Jabir, Hemedy Hamis, Suleiman Hemed, Abdulrahman Hassan, Salum Hemed, Alen Alex, Haudy Face na Hamis Gulam. Zoezi la kuchukua na kurudisha fomu katika kamati hiyo lilifikia tamati jana saa 10 jioni wakati uchaguzi mkuu utafanyika Desemba 8 mwaka huu mjini Dodoma. Wagombea wote watashiriki kwenye usaili utakaofanyika Jumanne ijayo jijini Dar es Salaam na wale watakaopita ndiyo watapata fursa ya kuchuana kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Desemba 8, mjini Dodoma.

Rais Chavez bado hoi kitandani

RAIS wa Venezuela Hugo Chavez anasemekana kuwa katika hali mbaya kutokana na matatizo yaliyotokana na upasuaji wa kumtibu saratani, ambao alifanyiwa nchini Cuba mwezi Desemba. Rais huyo mwenye umri wa miaka 58 anaendelea kupata nafuu katika hospitali moja mjini Havan na hajaonekana hadharani tangu alipofanyiwa upasuaji, ambao ni wa nne katika muda wa miezi 18. Chavez anatarajiwa kuapishwa kuchukua muhula mwingine wa uongozi wa miaka 6 baada ya kushinda uchaguzi mwezi Oktoba mwaka jana. Upinzani unataka aondoke madarakani kwa muda ikiwa ugonjwa wake utamzuia kula kiapo, kama inavyosema katiba ya nchi hiyo. Spika mpya wa Bunge la Venezuela Diosdado Cabello na makamu wa Rais Nicolas Maduro walisema wanaendelea kusimama pamoja na Rais Chavez. Hata hivyo inadaiwa kwamba kuapishwa rasmi kwa Rais Hugo Chavez wa Venezuela kwa kipindi kingine kipya cha miaka sita madarakani hapo tarehe 10 Januari kunaweza kuahirishwa iwapo kiongozi huyo anayetibiwa Cuba atashindwa kuhudhuria hafla hiyo. Makamu wa Rais Nicolas Maduro alisema kwamba Serikali ya Venezuela inapanga kuchelewesha hafla hiyo ya kumwapisha wakati ikijaribu kuepuka kumtangaza mtu wa kuchukua nafasi yake au kuitisha uchaguzi mpya katika nchi hiyo ya Amerika ya Kusini Mwanachama wa Nchi Zinazosafirisha kwa Wingi Mafuta Duniani (Opec). Kiongozi huyo wa Kisoshalisti mwenye umri wa miaka 58 ambaye amekuwa madarakani tokea mwaka 1999 hajaonekana hadharani kwa zaidi ya wiki tatu sasa. Washirika wake wanasema yuko katika hali mbaya kutokana na operesheni ya nne katika kipindi cha miaka miwili kwa saratani iliyoko kwenye fupa lake la nyonga ambayo aina yake haikutajwa. Upinzani wa kisiasa nchini Venezuela unasema kwamba kuendelea kwa Chavez kuwepo Cuba hapo tarehe 10 mwezi wa Januari ambapo inatajwa kuwa yu mahututi ni sawa na kujiuzulu kwa Rais huyo.

Kadi ya Bima ya Afya yazua utata jijini Dar

HOSPITALI ya Hindu Mandal, Dar es Salaam imeuzuia mwili wa Marystela Alfonce aliyefariki juzi baada ya kubainika kuwa alikuwa akitumia kadi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ya mtu mwingine aliyetajwa kwa jina la Honorata Magezi ili kupata matibabu. Hospitali hiyo jana ilikataa kutoa mwili wa marehemu Marystela hadi ilipwe Sh7.2 milioni ambazo ni gharama za matibabu tangu alipolazwa hospitalini hapo, Novemba 12, mwaka huu. Mwandishi wetu alishuhudia gari la kubeba maiti aina ya Marcedes Benz lililofika katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kuchukua mwili wa Marystela likiondoka bila kubeba mwili huo. Ilielezwa kuwa, marehemu alikuwa akitumia kadi ya ndugu yake kupata matibabu katika hospitali hiyo hadi kifo kilipomkuta. kutokana na tukio hilo, mume wa Honorata, Jovis Magezi anashikiliwa na polisi. Magezi ambaye ni Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, alikamatwa jana baada ya kufika Hindu Mandal kwa lengo la kuchukua mwili wa marehemu kabla uongozi wa hospitali hiyo na Bima ya Afya kushtuka. Daktari huyo alikamatwa baada ya maofisa hao kumbana kwa maswali. Mahojiano ya daktari huyo na kikosikazi hicho yalikuwa kama ifuatavyo: Ofisa wa Bima: Mna uhusiano gani na marehemu. Magezi: Ni mke wangu. Ofisa wa Bima: Mke wako alilazwa lini hapa hospitalini? Magezi: Wiki mbili zilizopita.

Askari JWTZ anaswa na pembe za ndovu Arusha

GARI aina ya Toyota VX linaloelezwa kuwa mali ya Serikali limekamatwa na polisi likiwa limebeba pembe za ndovu. Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa gari hilo lilikamatwa juzi saa 3:00 usiku katika Kijiji cha Kigongoni katika Mji wa Mto wa Mbu, wilayani Manyara baada ya gari hilo kupinduka. Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya Jeshi na Polisi zimeeleza kuwa askari wa jeshi hilo aliyekuwa akiendesha gari hilo anashikiliwa na polisi. Uchunguzi umebainisha kuwa ndani ya gari hilo kulikuwa na meno ya tembo na watu wengine watatu ambao walikimbilia porini na baadhi ya nyara hizo. Habari hizo zimedai bado kuna utata kuhusu gari lililokuwa likitumiwa na maofisa hao kwa kuwa kibao cha namba za gari hilo kinasomeka kwa namba za kiraia lakini vioo vimechorwa namba za Serikali, huku Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa akisema pia kulikuwa na namba za JWTZ. Kulingana na taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, kukamatwa kwa gari hilo kulitokana na Askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Hifadhi ya Ziwa Manyara kudokezwa na raia wema. Inaelezwa kuwa baada ya askari hao kudokezwa, walianza kufuatilia nyendo za maofisa hao ndani ya hifadhi na walipogundua wanafuatiliwa, gari hilo liliongeza mwendo kuelekea Mji wa Mto wa Mbu. Hata hivyo, kutokana na mwendokasi wa gari hilo na kutokuwa wazoefu kulinganisha na Askari wa Tanapa, gari la maofisa hao lilipinduka lilipofika Kijiji cha Kigongoni nje kidogo ya Mto wa Mbu. “Baada ya kupekuliwa lilikutwa na pembe mbili za ndovu na uchunguzi wa awali umethibitisha maofisa waliokimbia walifanikiwa kutoroka na pembe nyingine tatu,” kilidokeza chanzo hicho. Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kulitokana na wananchi kumtilia shaka yeye na wenzake gari lao lilipopata ajali kwa kitendo cha watu wawili waliokuwepo kwenye gari hilo kuonekana wakihamisha mizigo na kukimbilia porini. “Matairi mawili ya gari yalipasuka lakini ajabu ni kwamba wananchi walipojitokeza kusaidia majeruhi, wawili kati yao walinyanyua mizigo isiyojulikana na kukimbilia porini huku wakimwacha mwenzao aliyevaa sare za jeshi akisubiri garini,” alisema mtoa taarifa wetu. Kwa mujibu wa mashuhuda, wakati wa ajali hiyo, mtuhumiwa alikuwa amevaa jaketi la JWTZ pamoja na suruali ya jinsi akiwa na bunduki aina ya Rifle. Katika msako uliofanywa na polisi kwa kushirikiana na wananchi, pembe mbili zaidi za ndovu zilikutwa zikiwa zimefichwa karibu na eneo la ajali. Mkurugenzi mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini akasema hana taarifa kamili kwani yuko Tanga na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira. “Ni kweli nimearifiwa juujuu tu, nasubiri taarifa kamili lakini nimeambiwa tu hilo gari lilipinduka wakati wakifukuzana na askari wetu, lakini mnaweza mkapata taarifa zaidi polisi,” alisema Kijazi. Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema hajapata taarifa hiyo, hivyo asingeweza kutolea maoni kwa namna yeyote.

Wabunge waanza kujiandikisha JKT

WABUNGE vijana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameanza kujiandikisha tayari kwa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Mujibu wa Sheria kwa ajili ya mafunzo yatakayoanza Machi mwaka huu. Taarifa ambazo Mwananchi Jumamosi ilizipata juzi, zimeeleza kuwa, idadi ya wabunge ambao tayari wamejiandikisha kujiunga na JKT hadi sasa ni zaidi ya 31, huku wengine wakiendelea. Kujiandikisha kwa wabunge hao ili wajiunge na JKT kunafuatia wito uliotolewa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Julai mwaka uliopita, alipowasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake katika Bunge la Bajeti mjini Dodoma. Kwa nyakati tofauti wabunge vijana kutoka CCM, Chadema na NCCR- Mageuzi walilithibitishia gazeti hili kuwa tayari wamejiandikisha katika Ofisi ya Katibu wa Bunge kwa ajili ya mafunzo hayo. Imebainishwa kuwa, miongoni mwa wabunge waliojiandikisha, wamo pia ambao waliwahi kupitia mafunzo hayo, ikielezwa kuwa wamefanya hivyo wakitaka kwenda kujikumbushia. Hata hivyo, Kaimu Katibu wa Bunge, Eliakimu Mrema hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo akieleza kuwa linaweza kuzungumziwa na Spika wa Bunge kwa kuwa ndiye anayezungumzia masuala ya wabunge. “Sisi kazi yetu ni utendaji tu na masuala ya wabunge, Spika ndiye anayezungumzia,”alisema Mrema. Alipotakiwa kuzungumzia taarifa hizo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema kwamba ni mapema mno kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hawajapata idadi kamili. “Tukiwa Dodoma (bungeni), ukituuliza tutakuwa tayari kutoa taarifa kamili, lakini kwa sasa ni mapema kuzungumzia suala hilo,”alisema Ndugai na kuongeza: “Watu ni rahisi kusema, lakini wakati mwingine utekelezaji ni mgumu kama unavyosema kwani, ukisikia moja ya uamuzi mgumu, hili ni mojawapo.” Ndugai alisema kuwa mafunzo hayo hayatawahusu wabunge ambao waliwahi kupitia JKT siku za nyuma na kwamba ni maalumu kwa wabunge vijana. “Naomba usubiri Dodoma, tutakuambia hali ilivyo,” alisema Ndugai.

Moto wa gesi wazidi kushika kasi Mtwara

SAKATA la kupinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam limechukua sura mpya baada ya wananchi zaidi ya 30,000 kusaini katika fomu maalumu kupinga gesi hiyo kusafirishwa. Wakati wananchi hao wakikamilisha shughuli hiyo na kukabidhi fomu hizo kwa wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), umoja wa vyama tisa vya siasa mkoani umemwomba Rais Jakaya Kikwete kusitisha mradi huo ili kuepusha uvunjifu wa amani unaoweza kujitokeza. Pia, umoja huo umewataka wabunge wote wa Mkoa wa Mtwara kutangaza msimamo wa kila mmoja juu ya gesi kwenda Dar es Salaam au kukubaliana na uamuzi wa Serikali ili wajue nani msaliti kwao. Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Sabasaba mjini hapa, viongozi hao kwa nyakati tofauti wamemtaka Rais Kikwete kutokutumia ‘jazba na mabavu’ katika kulipatia suluhu jambo hilo, badala yake busara zitawale kwa kusitisha mradi huo. “Sisi Watanzania hatujazoea vita, bali tumezoea kupata hasara… katika hili naomba Kikwete akubali kupata hasara kama tunavyokubali hasara nyingine…Sisi wananchi tupo radhi tuingie kwenye deni kubwa kama hilo, lakini gesi haiwezi kwenda Dar es Salaam,” alisema Uledi Abdallah Makamu, Mwenyekiti wa umoja huo na kuongeza: “Hizo trilioni tatu kama anaona hawezi kuzilipa iwapo gesi itabakia Mtwara...Basi atafute njia nyingine za kulipa… Atambue kuwa hakuna fedha yenye thamani ya amani na utulivu wetu…akumbuke kuwa mafahali wawili hawakai zizi moja.”Naye Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mtwara Mjini, Mustafa Nchia aliwataka wabunge kutoa misimamo yao ili wananchi wajue ni mbunge yupi anawaunga mkono na yupi msaliti kwao. “Hadi sasa ni Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini), George Mkuchika, (Newala), Asnain Murji (Mtwara Mjini) na Clara Mwatuka (Viti Maalum CUF), wametoa misimamo yao, vipi ninyi wengine…Tunataka kusikia msimamo wa kila mmoja,” alisema Nchia huku akishangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo. Zitto ampinga Kikwete Wakati Rais Kikwete akisisitiza kuwa mgogoro kuhusu gesi unachochewa na wanasiasa kwa lengo la kukwamisha juhudi za Serikali za kumaliza tatizo la mgawo wa umeme, Mbunge wa Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amesema huo ni uzushi. Katika taarifa yake jana, Kabwe alisema Serikali haitashinda vita hii kwa kuzusha kwamba wanasiasa wanaopinga wanatumika na kampuni nyingine au kwa mataifa ya magharibi kutaka kuvuruga nchi. “Serikali ijitazame yenyewe. Bila kufanya hayo tunayo pendekeza, wananchi wataendelea kupigania haki yao...Hii ni vita ya uwajibikaji. Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za nchi yao. Kwa mujibu wa Zitto, Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na kuwatusi watu wa Mtwara, na kama ilivyozoeleka Rais Kikwete na mawaziri wake wamekuwa wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia umaarufu. “Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwaambia mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa yanayoendelea mkoani Mtwara yanachochewa na wanasiasa tuliosimama na wananchi wanaodai kufaidi utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na mawaziri wake wameshindwa kabisa kuonyesha uongozi katika suala hili na hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.” Aliongeza kuwa anafahamu kwamba Ubalozi wa China umeandika barua serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao. Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alifukuzwa na wananchi alipokwenda huko hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini?” alihoji. Waziri na wanasiasa Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene amesisitiza kuwa mgogoro na vurugu zinazoendelea mkoani Mtwara kuhusu gesi unachangiwa na wanasiasa. Alisema kuwa watu hao aliodai wanakosa uzalendo na utaifa, wanalenga kuhakikisha tatizo la umeme linaendelea kuwepo nchini hadi uchaguzi mkuu ujao ili wapate ajenda ya kisiasa jukwaani.