Kombe la Mapinduzi liamshe soka la Zanzibar

Tuesday, January 22, 2013

MICHUANO ya mpira wa miguu ya Kombe la Mapinduzi iliyoisha wiki iliyopita katika kilele cha sherehe za mapinduzi mjini Unguja katika uwanja wa Aman, kwa timu ya Azam FC kutetea taji imenipa mwanga mkubwa katika soka la visiwani humo. Kwa hakika nimeshuhudia soka la uhakika katika michuano ile hasa kutoka timu za visiwani, lakini katika kila timu wenyeji yaani za visiwani kulionekana kasoro moja tu ya uzoefu kwa wachezaji wake. Miembeni, Jamhuri ya Pemba ambao ndiyo mabingwa wa soka Zanzibar na Bandari ndiyo timu wenyeji zilizoshiriki michuano hiyo. Lakini Miembeni ndiyo iliyofanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ikitolewa na Tusker FC ya Kenya. Kwa soka waliloonyesha Miembeni na Jamhuri ya Pemba nimevutiwa kutaka kuwaona wakiendelea zaidi na zaidi. Maana ya maneno haya ni kuwashawishi viongozi wa timu mbili hizi kuomba mechi nyingi za kirafiki na timu za Tanzania Bara ima kwa kuzialika au wao kuzifuata kila msimu wa ligi kuu unapoisha. Nimefuatilia kwenye kumbukumbu nimeona Miembeni ni timu kongwe kuliko hata baadhi ya timu zinazoonekana bora katika ligi kuu ya Tanzania Bara, Miembeni ilianzishwa mwaka 1945. Katika mafanikio yao tangu kuanzishwa Miembeni walishachukua ubingwa wa ligi kuu Zanzibar mwaka 1987, 2007 na 2008. Halafu katika kombe la Mwalimu Nyerere wamechukua mara tatu mwaka 1985, 1986 na 1987. Kikombe cha Mapinduzi wamechukua mara mbili mwaka 2008 na 2009. Aidha Miembeni FC walishiriki kombe la shirikisho (CAF) mwaka 2010, wakashiriki kombe la mabingwa barani Afrika (African Cup Winners) mwaka 1986, 1987 na mwaka 1988. Si mafanikio madogo kwa timu ambayo watu wengi hawaijui ama wanaijua lakini hawaitilii maanani. Timu ya pili kutoka visiwani humo ambayo ilinivutia ni Jamhuri ya Pemba, hawa ni mabingwa wa ligi kuu Zanzibar kwa msimu uliopita mwaka 2012. Ilianzishwa mwaka 1953 ikiwa na makazi yake mjini Wete Pemba. Wao wamechukua Kombe la Mapinduzi mara moja yaani mwaka 1998, na mwaka 2012 walifika fainali wakafungwa na Azam FC. Jamhuri ya Pemba iliushangaza umma kwa kuifunga Mtibwa Sugar magoli manne kwa moja (4-1) katika mechi ya ufunguzi wa kundi B michuano ya Mapinduzi iliyomalizika juzi. Ina kikosi bora kinachoweza kuleta ushindani katika soka la Afrika, lakini macho mangapi yanashuhudia uwezo huo? Lengo la makala haya ni kuwafungua macho viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kuzitangaza zaidi timu zao kwa kupitia michuano mikongwe kama hii ya Mapinduzi. Historia inaonyesha mwisho wa michuano ya Mapinduzi wachezaji wa timu za Zanzibar wanaishia kuchukuliwa na timu zilizoalikwa. Hiyo si sifa wala jambo la kujivunia maana kuchukuliwa wachezaji ina maana moja tu ambayo ni kudhoofisha soka la Zanzibar. Vijana wa Zanzibar wanapenda kucheza soka, lakini wanaonekana kurudishwa nyuma na mifumo mibovu ya viongozi wao. Suala la viwanja bora vyenye viwango na mikakati ya vyanzo vya mapato kwa timu hizo ni kitu cha kuzingatia sana. Dunia sasa inaendeshwa kwa ujasiriamali katika michezo, biashara nyingi zinatangazwa na vilabu vya mpira wa miguu. Uchumi wa Zanzibar unaweza kukua kwa kutegemea soka ikiwa wataweka mbele malengo ya wachezaji wao.

No comments:

Post a Comment

Tuachie Ujumbe wako hapa .