2013 muziki wa kizazi kipya uwe wa ubunifu zaidi

Tuesday, January 22, 2013

SANAA ya muziki Tanzania imekuwa ikikua siku hadi siku. Moja ya viashiria vya kukua kwa muziki ni kuibuka kwa wanamuziki kila kukicha ambao wamekuwa wakija na staili tofauti kwa lengo la kukamata soko la ndani na nje ya nchi. Kuna waliofanikiwa kufanya vizuri na kukamata soko la ndani na nje na kufanya mambo muhimu na hata kutengeneza mazingira ya kutoa ajira kwa Watanzania wenzao. Lakini pia kuna walioishia katika soko la hapa nyumbani na hakuna lolote la maana walilofanya zaidi ya kulewa sifa na umaarufu. Halikadhalika kuna walioshindwa kutimiza ndoto zao katika fani hii ya muziki lakini bado wanaendelea kujaribu bahati yao. Moja ya aina ya muziki ambao umekuwa unajaribiwa na wengi na hasa vijana ni ule muziki wa kizazi kipya, maarufu kama Bongo fleva. Kwa wale wapenzi wa burudani ya muziki watakubaliana na mimi kuwa aina hii ya muziki imekuwa ya majaribio kwa kila kijana ambaye anajisikia kuwa anaweza kuingia katika tasnia ya muziki. Hivi karibuni tumeshuhudia hata watu wazima wenye umri wa miaka zaidi ya 50 nao wakitupa karata yao katika aina hiyo hiyo ya muziki. Haya yote yamefanyika na kweli wapo waliofanikiwa kuufanya muziki wa Bongo fleva vizuri kwa kujipatia mashabiki wengi na hatimaye kupata soko. Katika miaka ya nyuma wanamuziki wa Bongo fleva walikuwa wanaweza kufanya maonyesho mengi zaidi ikiwepo yale ya uzinduzi wa albamu tofauti na ilivyo sasa. Kinachofanyika sasa hivi katika muziki wa kizazi kipya ni wanamuziki kufanya nyimbo zao kwa kushirikishana. Hali hii ambayo inatafsiriwa kama njia ya kutafuta soko na umaarufu kwa nguvu inafanywa zaidi na wale wanamuziki wanaochipukia kwa kuwashirikisha wale wakongwe na hasa wenye majina makubwa. Kwa harakaharaka, tafsiri yake ni kwamba wanamuziki wanaochipukia kwa sasa katika muziki wa kizazi kipya hawawezi kusimama wenyewe na kuleta mabadiliko bali wameona njia pekee ya kulazimisha soko ni kuwashirikisha wanamuziki wenye majina makubwa. Hii ni mojawapo ya viashiria kwamba kumbe muziki wa kizazi kipya hauna ubunifu kama ilivyo katika aina nyingine ya muziki kama vile dansi na nyinginezo. Kuna wanamuziki waliokuwa wakipiga Bongo fleva zamani na sasa wamegundua kuwa muziki huo sasa hauna jipya na sasa wameamia katika staili nyingine na pia wengine wameamua kuanzisha bendi zao ili kupiga muziki wenye ladha tofauti. Huu ni uamuzi mzuri ambao unakwenda na wakati na hasa katika karne hii ambayo imejaa uvumbuzi na ushindani wa kila aina. Kuna kundi jingine la wanamuziki wa muziki wa kizazi kipya ambao wamepotea katika macho na masikio ya wadau wa muziki japokuwa waliwika sana enzi hizo. Aidha pia kuna wale ambao ubunifu wao ni kama umefika kikomo na kilichobakia ni kupata mashabiki kwa sababu wana mvuto kwa wapenzi wa muziki wa aina hiyo, na hii ni kwa sababu kila wakipanda majukwaani nyimbo wanazoimba ni zile zile za miaka nenda rudi. Hili nalo limeleta mjadala kwani kuna wanaothubutu kusema kuwa bora Bongo fleva ya zamani ni bora kuliko ya sasa. Wanaosema haya wana sababu kuu ya msingi ya kwamba Bongo fleva ya sasa haidumu sokoni kama ilivyokuwa ya miaka ile kwa sababu wasanii wa sasa hawawezi kufanya muziki bila kuwashirikisha wasanii maarufu. Kwa maana hiyo ni kwamba kama wasanii wanaochipukia watashindwa kusimama imara hakutakuwa na jipya katika Bongo fleva kwa miaka ijayo. Mfano mzuri ni katika mojawapo ya onyesho la Krismasi lililofanyika wiki iliyopita katika moja ya kumbi maarufu za jijini Dar es Salaam. Katika onyesho hilo kulikuwa na wasanii wa muziki wa Bongo fleva wa sasa na wa zamani. Kilichotokea ni kwamba wale wanamuziki wa sasa na wale wakongwe wa Bongo Fleva wote walipokelewa kwa shangwe sawa na mashabiki waliokuwa wamefurika katika ukumbi huo. Halii hii ilitafsriwa kama ule usemi usemao kuwa ‘Ya kale ni dhahabu.’ Hii ikiwa na maana ya kwamba bado wanamuziki wakongwe katika Bongo fleva wana nafasi kubwa ya kukubalika kuliko wa sasa. Tatizo kubwa la wanamuziki wa sasa wamelewa sifa na umaarufu na wengine kutumia nafasi hiyo kuendekeza mapenzi kwa kubadilisha wasichana kama nguo. Hawa nao wamejisahau bila kujua kuwa kuna wasanii wengi wa tabia kama hizo walishapita na sasa wana maisha magumu na kilichobaki masikioni mwa watu ni historia tu. Mwaka 2013 uwe wa mabadiliko kwa wanamuziki wa Bongo fleva kwa kuja na ubunifu zaidi kwa sababu kwa sasa hali ilivyo Bongo fleva ni kama Big G inayotafunwa na baadaye kuisha utamu. Ni muziki ambao unadumu kwa muda mfupi na kupotea kabisa katika macho na masikio ya mashabiki. Sababu kubwa ni wasanii kutojiandaa kabla ya kutengeneza nyimbo zao. Tabia hii ya wasanii wa Bongo fleva ya kufanya nyimbo zao bila kujiandaa imewaingiza katika wimbi la kuiga, yaani Kukopi na kupesti. Hali inaonyesha kuwa wanapenda njia ya mkato zaidi kuliko kubuni stahili zao. Wanamuziki wa Bongo fleva sasa wamekumbwa na upepo wa Afrika Magharibi na Afrika Kusini. Hali hii ya kuiga imetawala sana katika mwaka 2012 ambapo tumeshuhudia wanamuziki wengine wakipata tuzo za ubora kutoka kwa waandaaji wa mashindano mbalimbali ya muziki. Hali hii pia ilileta maswali mengi kwa waandaaji wa tuzo hizo, swali kubwa likiwa ni kwamba ni vigezo gani wanavyovitumia kupata washindi wa tuzo hizo. Tabia ya kupenda kuiga bila kujifunza pia imeshuhudia wanamuziki wetu wakijaribu kuimba nyimbo zao moja kwa moja kwa kufuatisha vyombo majukwaani, lakini bado kiwango chao kinaonekana kuwa ni cha kuchechemea au dhaifu. Mfano mzuri ni katika mojawapo ya tamasha kubwa la muziki ambalo limekuwa likifanyika kila mwaka katika sehemu mbalimbali hapa nchini na kujizolea umaarufu. Mwaka jana Nilishuhudia wanamuziki wa muziki wa Bongo fleva wakijaribu kuimba na vyombo, yaani Live. Kwa wale wanaofahamu uimbaji wa staili hiyo watakubaliana na mimi kuwa vijana hao ambao ni maarufu katika muziki wa Bongo fleva kuwa ‘walichemka’ hivyo kuwashangaza watu wengi. Ndiyo, kujaribu kufanya kitu anachofanya mwenzio si vibaya, lakini pia kabla ya kujaribu ni vyema kufanya maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti za hapa na pale kufahamu kuwa wale ambao walifanya hivyo na kufaulu walitumia njia zipi hadi kufikia mafanikio. Wanamuziki wa Bongo fleva hawanabudi kutambua kuwa kuteleza siyo kuanguka, kwa hiyo bado wana nafasi ya kuangalia ni wapi wameteleza na kujirekebisha na hatimaye kufanya vizuri zaidi. Nina imani kuwa kuna Watanzania wengi ambao wangependa kuona mabadiliko katika muziki wa kizazi kipya kuliko kuona kila siku wakiiga staili kutoka nchi za Magharibi ambazo mwisho wa siku zitachangia kumomonyoa maadili yetu na kufunika utamaduni wetu. Wanamuziki wa Bongo fleva kama walivyo wasanii wengine, wana haki ya kutangaza utamaduni wao kama mojawapo ya wajibu wa msanii wa aina yoyote ile. Mwaka 2013 Bongo fleva iwe ya ubunifu zaidi na hili bado linawezekana.

No comments:

Post a Comment

Tuachie Ujumbe wako hapa .