Ukuta waharibu magari 19 Ubungo

Tuesday, January 22, 2013

UKUTA wa kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo jijini Dar es Salaam (UBT), umeanguka ghafla na kujeruhi watu wanne huku magari madogo 19 na pikipiki za matairi matatu (bajaji) vikiharibika vibaya. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha tukio hilo akisema kuwa lilitokea alfajiri saa 12 jana, kutokana na ukuta huo kuelemewa upande mmoja baada ya kubomolewa upande mwingine. Kenyela alisema hakuna aliyepoteza maisha, isipokuwa watu wanne walijeruhiwa na kupatiwa matibabu hospitalini, na juhudi za kutoa magari hayo zilikuwa zikiendelea. Magari yaliyoharibika yalikuwa yameegeshwa jirani na ukuta huo na watu waliokuwa wamewasindikiza ndugu zao kupanda mabasi kituoni hapo. Hata hivyo, pamoja na ukuta huo kubomolewa upande mmoja juzi, uongozi wa kituo hicho haukuweka alama yoyote ya kuwatahadharisha watembea kwa miguu wala wenye magari wasisogelee eneo hilo. Kwa mujibu wa kamanda Kenyela, magari yenye bima wamiliki wake watarudishiwa gharama zote baada ya kufanyiwa tathmini. Nao mashuhuda wa tukio hilo, waliliambia Tanzania Daima kuwa chanzo ni uzembe wa mkandarasi pamoja na meneja wa kituo hicho. Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika eneo la tukio, wananchi hao walisema kuwa serikali inapaswa kulaumiwa kwa kutofanya maandalizi ya kutosha kabla ya kubomoa. Mashuhuda hao walisema kuwa licha ya ujenzi kuendelea, askari wa wanaolinda humo ndani walikuwa wakiendelea na utaratibu wa kutoza fedha za maegesho na kuwaelekeza madereva eneo kuegesha eneo hilo la ukuta. Naye meneja wa kituo hicho, Idd Juma, hakutaka kuzungumza chochote kwa madai kuwa si msemaji na hivyo kutaka asubiriwe mkurugenzi wa manispaa hiyo. Akizungumzia ajali hiyo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema wakati hatua za kisheria zikitakiwa kuchukuliwa haraka kutokana na uzembe uliosababisha tukio hilo serikali kuu inapaswa kuingilia kati kuepusha maafa zaidi. Akizungumza kituoni hapo, Mnyika alisema ajali hiyo ya kizembe ni matokeo ya udhaifu wa serikali kutochukua hatua kwa wakati, hivyo inatumia utaratibu mbovu kukihamisha huku kikiendelea kutumika. “Tangu 2011 niliishauri serikali, ikiwemo kupeleka hoja binafsi kwenye Baraza la Jiji, ambapo pamoja na masuala mengine, niliitaka kufanya maamuzi ya haraka kuainisha mapema maeneo ya kituo cha basi Ubungo, ambayo yatatumia mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART),” alisema. Alisema kuwa kwa mwenendo huo wa kuitegemea menejimenti ya kituo kutokana na sh milioni 5 inayokusanya kila siku hapo, hawatamaliza kujenga hicho kituo mapema, hivyo wito kwa Rais Jakaya Kikwete ili fedha zitoke kituo kipya kijengwe.

No comments:

Post a Comment

Tuachie Ujumbe wako hapa .