Watanzania watakiwa kujenga hoteli za kitalii

Wednesday, March 20, 2013

Mh Nyalandu


WAJASIRIAMALI nchini, wametakiwa kujenga hoteli za kitalii kwa lengo la kukabiliana na tatizo kubwa la uhaba wa vitanda katika hoteli hizo.
Naibu Waziri wa Maliasilia na Utalii, Lazaro Nyarandu alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati akizundua hoteli ya kitalii ya Palace ambayo imejengwa kwa ubia na Shirika la Nyumba Nchini(NHC).
Lazaro alisema uwekezaji huo utasadia kuongeza idadi kubwa ya watalii na  mapato nchini.
“Mwaka jana tulipata watalii 800,000 ukilinganisha na Rwanda ambayo ilipata 600,000 licha kuwa nchi ndogo,  tatizo kubwa la nchi yetu ni upungufu wa vyumba vya kulala wageni,”alisema Nyarandu.
Alisema ujenzi huo utasaidia Mkoa wa Arusha kuongeza idadi ya vitanda vya kisasa vya kulala wageni. Mkoa wa Arusha sasa una  jumla ya vitanda 2,800  tu, nyuma ya Mkoa wa Dar es salaam wenye vitanda 3,800 wakati Mkoa wa Mwanza una vitanda 900 licha ya ukubwa wake.
“Tunaomba shirika la nyumba lijitanue kwa kujenga hoteli za kisasa za kitalii, sisi wizara tunahitaji wawekezaji wa ndani na nje wajitokeze kujenga katika maeneo ya wazi na ndani ya hifadhi zetu, tumejipanga kukabiliana na watumishi wanaokwamisha watu wenye nia njema,”alisisitiza.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu  alisema ujenzi wa hoteli hiyo yenye hadhi ya nyota nne, umegharimu Sh16 bilioni na NHC imetoa ardhi na Sh9 bilioni huku kiasi kingine kikitolewa na Palace Hoteli.
Alisema mradi wa hoteli hiyo ni moja ya miradi ambayo imekuwa na manufaa makubwa, kutokana na uwazi wa kuendesha hoteli hiyo na hivyo kuingiza mapato kwa pande zote NHC na mbia.
Naye Dk Macha alisema mradi huo hadi sasa umetoa ajira kwa wafanyakazi 120 na unatoa huduma nyingine kadhaa, ikiwamo huduma za kibenki na utachangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Mkoa wa Arusha na Taifa.
Akifungua mradi huo rasmi, Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka alipongeza mradi huo na kutoa wito kwa wajasiriamali kujitokeza na kuingia ubia na NHC katika kutekeleza miradi mbali mbali.
Alisema mradi huo unakwenda vizuri na umeongeza mapato ya NHC kwani katika eneo hilo, kabla ya ujenzi wa hoteli walikuwa wakipata kwa mwaka Sh31 milioni pekee, lakini sasa wanapata Sh151 milioni.

No comments:

Post a Comment

Tuachie Ujumbe wako hapa .